Thursday, 2 June 2016

FASIHI SIMULIZI NI MFUMO TIMILIFU KATIKA MAKUZI YA BINADAMU TANGU KUZALIWA KWAKE HADI KIFO.


FASIHI SIMULIZI NI MFUMO TIMILIFU KATIKA MAKUZI YA BINADAMU TANGU KUZALIWA KWAKE HADI KIFO. 


BY KIWALE BRASTO, FESTO.
© 2016, IRINGA, Tanzania
RUAHA CATHOLIC UNIVERSITY
Kiwale Company Publishers



USULI/ Dhana ya fasihi simulizi
Fasihi simulizi ni utanzu wa fasihi ambapo unawakilisha sanaa ya lugha unaopitishwa kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno au masimulizi ya mdomo. AU

fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia mdomo (tofauti na maandishi kama ilivyo fasihi andishi) ili kufikisha ujumbe. Au ni kazi ya sanaa inayotumia mazungumzo ya ana kwa ana ikihusisha utendaji na njia nyingine za mawasiliano kama vile Tape rekoda, redio na runinga ili kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Makuzi ni namna mtu anavyolelewa au malezi. Malezi au ulezi ni mafundisho au uangalizi (Mohamed, 2002).
Makuzi na fasihi katika jamii ambayo binadamu anaishi  hupitia hatua mbalimbali, Katika hatua hizo ndipo hukutana na fasihi, kwani ndimo ambamo fasihi inapatikana. Fasihi kama chombo cha kuelimisha, kuonya na kukosoa jamii basi humsaidia binadamu katika makuzi yake.
Hivyo basi, katika hatua hizo za makuzi ya binadamu hukutana na fasihi kulingana na rika alilonalo. Kwa mfano,Fasihi katika rika la watoto kuna michezo ya watoto, fasihi katika rika la ujana kuna methali, fasihi katika utu uzima kuna hadithi na fasihi katika kifo kuna Hotuba za misibani ambazo zinaelezea wasifu wa marehemu.

Fasihi katika rika la utoto
Makuzi ya watoto hutegemea malezi na matendo yanayofanywa na wazazi, walezi na hata jamii kwa ujumla yote haya hufanikiwa kupitia katika tanzu za fasihih simulizi.
Nyimbo za watoto kama vile pembezi, nyimbo hizi hutumika kubembeleza watoto ili walale (Mlokozi, 1996: 64).
                                    Lala mtoto lalax2
                                                Mama anakuja lala x2
                                                                        Anakuletea ndizi lala x2
                                                                        Usingizi wa mama uje hapa x2
                                                                        Usingizi wote wa baba uje hapa x2
 Pia zipo nyimbo  kama vile “maua mzuri yapendeza” and “mama nipe maji” huwaandaa watoto kukua kihaiba kwa kupenda usafi wa miili na mazingira yanayo wazunguka, kwani nyimbo hizi zinasisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na kuoga pindi anapotaka kwenda shule.Pia fasihi simulizi huwafunza watoto ubunifu na kukua kiakili, mathalani michezo ya watoto kama vile “Ukuti ukuti” na “Namtafuta mke wangu” .
Kupitia michezo hii huwafanya watoto kuwa wabunifu wa kutatua matatizo pindi wachezapo michezo, vilevile huwafunza watoto wa kike na kiume huigiza majukumu ya kifamilia kama vile kushirikiana,pia ipo michezo mingine kama “kibaba baba na kimama mama” ambayo huwafunza watoto majukumu katika jamii zao kama vile kukamua maziwa, kuandaa chakula, kulea watoto, kuchota maji na kuchanja kuni.

Fasihi  katika rika la ujana
Katika hatua ya ujana binadamu anaanza kujiingiza katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa kufuata utaratibu wa jamii husika. Fasihi simulizi inahitajika kwa kiasi kikubwa katika kuwalea vijana na kuwaweka katika mila, taratibu na maadili yanayokubalika na jamii.Fasihi simulizi katika makuzi ya vijana ni kama ifuatavyo;
Kupitia simo au misimu ,methali, nyimbo na hadithi, hutumika kuwaasa na kuwaonya vijana kuwa na maadili mema. Kwa mfano vijana wanapokuwa katika vijiwe vyao vya maongezi hutumia misimu na semi katika kupamba mazungumzo yao ili wajitofautishe na kundi linguine kama wazee au watoto (Ndugo na mwenzake, 1993). Mfano, Dude, Chura, Mkia, Msambwanda, Inye ndembendembe plus zote zikiwa na maana ya mwanamke mwenye makalio makubwa.
Pia zipo methali zitumikazo katika rika hili mfano usione vyaelea ujue vimeundwa,mtaka cha uvunguni sharti ainame,Asiyesikia la mkuu huvunjika guu,Mtoto akililia wembe mpe. Mkaidi hafaidi mpaka siku ya idd.
Methali hizi bila shaka zinatumika katika mazingira ya kumuonya na kumkanya kijana mkaidi kuhusu hatari ya jambo baya analokusudia kulifanya. Hivyo zinawalea vijana katika maadili yenye matokeo chanya kwao (Mlokozi, 1996: 36).
Vile vile kupitia hadithi  huweza kusaidia makuzi ya vijana mfano hadithi  ya “Abunusi’ inahusu kijana mwelevu anayejifanya mjuaji wa kila kitu ambayo huwaasa vijana wawe wanawasikiliza wenzao
Hata hivyo vitendawili, kwa kuangalia vipera vyake kama mafumbo na chemsha bongo, fasihi simulizi huwajengea vijana uwezo kwa kufikiri katika kutambua, kuhusisha, kulinganisha na kutofautisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika mazingira yake. Kwa mfano,Namsikia tu wala simujui na simuoni- Mwangwi. Kuku wangu katagia mibani- Nanasi. Ameingia shimoni akiwa uchi ametoka amevaa nguo mpya- Karanga.
Mfano wa chemsha bongo;Nina kilo moja ya manyoya na kilo moja ya mchele. Je kipi kina uzito zaidi? - Vyote vina uzito sawa. Mzee kudura alikuwa na kuku, mbele ya kuku huyo palikuwa na kuku na nyuma ya kuku palikuwa na kuku, Je mzee alikuwa na jumla ya kuku wa ngapi? - jibu Wawili (Ndande na ikambili, 1991: 96 katika Mlokozi, 1996: 41).
Chemsha bongo hizi mbili zinaimarisha uwezo wa kufikiri wa kijana kwa kuwa zinamtaka atumie akili na ujuzi mwingi ili apate jibu.
 Vile vile Kuna Nyimbo zinawakumbusha vijana kuwaheshima na kuwathamini wazazi na watu wengine. Kwa mfano, Msanii Jumanne Idd katika wimbo wa “baba na mama” anaimba yafuatayo;
            Angalia maajibu ya dunia, mitihani Mungu aliyotutolea,
                Baba na mama ni nguzo ya dunia, ikianguka ujue umeangamia,
                Kwa nini sawa na bibi kwenye maji, inaelea imekosa mvushaji,
                Hata kama tajiri hauna kipaji, mchango wa wazazi utauhitaji.
Ikiwa unawanyanyapaa wazazi, yaani huwaheshimu wazazi unadiriki kuwafanya
vijakazi nakuapia wewe utapata radhi kwani bila wewe nisingekuwepo.
Hali kadharika fasihi simulizi kupitia nyimbo hutumika kutoa hamasa na ari kwa vijana kufanya kazi kwa bidii huku akiweka kando uvivu. mfano ,wimbo kutoka kwenye kabila la wabena
                                                            Iligimilo ni nyengox2
                                                                                                wote
                                                                                Ye dadoho nu nyohox2
                                                                Ukangalage ulimage, tilaliya humwahax4    
Wimbo huu una maana ya kuwa “jembe na mundu, ndiyo baba yako na mama yako, ukazane kulima tutakula mwakani”
Pia utanzu huu wa wimbo hutoa burudani kwa vijana  kwa sababu burudani ni sehemu ya maisha. Mfano, nyimbo za bongo fleva, wimbo wa “bado” ulioimbwa na Harmonizer na Diamond Platinumz.

Fasihi katika rika la uzee (utu uzima),
Uzee ni kipindi ambacho mwanadamu hupitia katika maisha yake ,kipindi hiki kinanzia miaka 50-80 na kuendelea  katika kipindi cha uzee fasihi husaidia katika
 Husaidia kuwalea watoto wao au vijana katika makuzi bora kupitia methali na nahau mfano mchelea mwana hulia kulia yeye, mvumilivu hula mbivu, kuishi kwingi kuona mengi
Fasihi simulizi huwafanya wazee kuthamini tamaduni zao mfano sala za matambiko, kupitia matambiko haya jamii hujifunza tamaduni zao.
Fasihi simulizi huwaburudisha wazee kupitia malumbano ya watani na michapo.

Fasihi na kifo
Fasihi kama amali ya jamii haikuacha kuzungumzia suala la kifo kwani hii ni hatua ya mwisho ya makuzi na maisha ya binadamu. Katika kuonesha suala hili zipo tanzu na vipera mbalimbali vya fasihi ambazo hufanya kazi mahususi katika jamii iliyofikiwa na kifo (kuondokewa na mpendwa wao) na utokeaji wa tanzu hizi uko katika sehemu tatu nazo ni kama zifuatazo;
Wakati wa kutangaza na mkusanyiko wa ndugu (watu). Katika wakati huu zipo tanzu anuai ambazo hufanya watu kukubaliana na hali iliyotokea na upo utaratibu maalumu wa utoaji taarifa kutoka jamii moja na nyingine na hata kuwafariji wafiwa. Tanzu hizo ni kama methali, nahau, nyimbo na semi. Mfano,Poleni ndugu zetu, kazi ya Mola haina makosa, Mbele yake nyuma yetu. Hakuna chenye mwanzo kisicho na mwisho,
 Pia zipo mbolezi mbalimbali katika hatua hii. Mfano;
                                                Parapanda italia parapanda italiaX4
Wakati wa kuaga na matayarisho yake (upambaji na uoshaji). Hiki ni kipindi ambacho marehemu anatakiwa kuagwa na hutayarishwa kwa kuzikwa. Katika hatua hii pia zipo tanzu mbalimbali za fasihi ambazo huwakumbusha tukio. Mfano sala, maigizo ya watani na malumbano yao. Hapa jeneza hutolewa nje na baadhi ya viongozi wa kimila na kidini humuombea marehemu kwa kutumia lugha maalumu.
Pia watani nao huiga tabia, mavazi na matendo ya marehemu ili kuonya na kuliwaza wafiwa. Utani huu unaweza kuwa wa kabila na kabila au wajukuu. Mfano katika kabila la wandamba, wapogoro, wandwewe na wangindo huwa hawalii au hulia kwa kejeli kwa wazazi wao kwa kifo cha bibi zao na babu zao. Pia hudai kuku kama furaha.
Wakati wa maziko, hapa hujumuisha kazi za fasihi kama vile hotuba na kumbukumbu huandaliwa na kusomwa mbele ya jamii ili kutoa wasifu wa marehemu. Mfano hotuba hiyo ni;
            Marehemu sada adamu, alizaliwa mwaka 1940.
            Marehemu alijaaliwa kuwa na watoto 70, wajukuu 120 na wake 32
            Ndugu sada aliwahi kuajiliwa katika Kampuni ya MATOZ CLASSIC na alitumikia kazi hiyo kwa muda wa miaka 30.
Mwisho marehemu alifariki kwa ugonjwa wa kisukari baada ya kuanguka ghafla akiwa kazini na tunatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi.

Hivyo basi Fasihi simulizi imekuwa kama mama katika malezi na makuzi ya mwanadamu, kwani kupitia fasihi simulizi binadamu katika rika zote hujifunza vitu vipya ambavyo humsaidia katika kutatua changamoto mbalimbali za kimaisha za kila siku.

No comments:

Post a Comment