NADHARIA ZINAZOELEZEA CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI/MASIMULIZI
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika sehemu hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Tukianza na fasili ya Nadharia, Massamba (2009:63) anasema, nadharia ni taratibu kanuni na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea jambo. Sarantakos (1997: 9) amefasili nadharia kama jambo linalofanywa na kuthibitishwa kwa utaratibu maalum kwa njia ya utafiti kwa ajili ya kuelezea jambo fulani katika jamii. Martin E. Amini (2005:10) anasema nadharia ni jumla ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia kuelezea, kuchambua, kuelewa au hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalum.
Hivyo basi, nadharia huchukuliwa kama dira au muongozo wa kumuongoza mtafiti/mchambuzi ili kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo unaotarajiwa kuwa imara zaidi kuliko mtazamo mwingine. Hivyo tunaweza kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi simulizi ni chombo kinachotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani.
Maana ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema, ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei (2005:65) anasema ngano kuwa ni hadithi fupi na zenye masimulizi yasiyo ya kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W. (2003:165) anasema ngano ni hadithi ya kale ambayo ni moja kati ya tanzu maarufu za fasili simulizi. Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na mwanzo wa hapo zamani za kale.
Kwa fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Baada ya kuangalia fasili mbalimbali za nadharia na ngano, sehemu inayofuata ni kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Tukianza na Okpewho (1992) ameanisha aina sita za nadharia zinazoelezea asili ya fasihi simulizi/masimulizi ambazo ni, nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya uamilifu, nadharia ya urasimi, nadharia ya Saikochanganuzi na mwisho ni nadharia ya Umuundo. Kwa upande wake, Miruka (1994) ameanisha aina tano za nadharia ambazo ni, nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya urasimi, nadharia ya uamilifu na nadharia ya umuundo, wakati Finnegan (1970) ameanisha aina tatu za nadharia ambazo ni nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya Umuundo.
Tukiangalia uanishaji wa nadharia hizo za wataalamu hapo juu, tunaona kuwa, wataalamu hao wanatofautiana katika idadi ya nadharia hizo, lakini kimsingi wataalamu wote wanakubaliana kuhusu nadharia fulani fulani, mathalani, wote wanakubaliana uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo. Lakini Okpewho na Miruka wanakubaliana juu ya uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo, nadharia ya urasimi na nadharia ya uamilifu. Okpewho anainisha aina nyingine ya nadharia ya Saikochanganuzi ambayo haijitokezi kwa hao wataalamu wengine. Hivyo katika uwasilishaji wetu, tutazigawa nadharia hizo katika aina sita kama ifuatavyo:
Nadharia ya wanamabadiliko, nadharia hii iliasisiwa na Charles Darwin ambaye alikuwa mwana bailojia karne ya 19, alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe ambao waliishi miaka mamilioni iliyopita. Katika utafiti wake aligundua kuwa viumbe walioendelea kuishi imewezekana tu kwa sababu ya kumudu mapambano dhidi ya uhaba wa vyakula, hivyo Darwin aliita jambo hili kama “Uhai kwa wanaofaa”. Pia aligundua viumbe walioendelea kuishi kwa sababu ya maumbo yao na mazingira yaliyosababisha wao kuwepo.
Mawazo ya utafiti wa Darwin yalishadadiwa na wanazuoni mbalimbali waliokuwa wanachunguza utamaduni wa binadamu, katika utafiti wao walikusanya simulizi kutoka jamii mbalimbali za Afrika, Asia na Amerika ambapo baada ya kukusanya simulizi hizo waligundua zilikuwa na ufanano wa kimaudhui. Wanamabadiliko wanaamini kuwa ngano/masimulizi tuliyonayo leo yana asili moja isipokuwa zimekuwa zikibadilika kutokana na mabadiliko ya wakati. Zaidi ya haya wanamabadiliko wanaamini kuwa viumbe wote tumetokea kwenye asili moja hivyo tuna uwezo wa akili sawa na maendeleo tutakuwa sawa.
Ubora wa nadharia hii, nadharia hii ndiyo msingi wa nadharia nyingine zilizofuata kama nadharia ya msambao, urasimi na uamilifu. Vilevile imesaidia kuelezea asili ya ngano/masimulizi hasa ngano zinazofanana kimaudhui, na mwisho nadharia imesaidia kuonesha kuwa ngano zina asili moja isipokuwa zinabadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mazingira.
Mapungufu ya nadharia hii, wanamabadiliko waliamini kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi kilihesabika kama masalia ya zamani/mabaki ya fasihi zilizotangulia, kwa maana kwamba kila kitu kilichosalia kitakuwa na dosari hakiwezi kuwa kitu halisi. Wanamabadiliko pia wameangalia tu upande wa maudhui na kuacha kipengele cha fani kama vile muundo na mitindo ya fani husika. Mwisho, pamoja na ufanano wa huo wa kimaudhui kuwa ngano zina asili moja lakini kuna tofauti kubwa hasa katika utendaji wa fanani hivyo fanani hutofautiana.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inahusiana na ngano za Kiswahili katika sanaa za jadi ambayo ni elimu inayohusu asili ya binadamu pamoja na umuhimu wake ambao ilihusishwa na usimulizi wa ngano ambayo ilitokana na jamii husika katika shughuli mbalimbali za jamii kama vile jando na unyago, miviga, vyanzo vya vyakula, sherehe, matambiko kwa kutaja kwa uchache.
Nadharia ya msambao, nadharia hii imeasisiwa na wataalamu kama Jacob na Wilhem Grimm, baadaye mawazo yao yaliendelezwa na Maxmuller na Mmarekani Stere Thomson. Pamoja na kwamba kulikuwa na tofauti ndogondogo lakini wataalamu wa nadharia hii wanamwelekeo mmoja ambao wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni moja lakini kutokana na maingiliano ya kijamii ndiyo yaliyosababisha kusambaa kwa hii ngano hasa kutoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) kuja katika jamii zisizostaarabika (Afrika).
Okpewho anasema, wanamsambao walijishughulisha na kuhusianisha ngano za jamii mbalimbali na kugundua kuwa ngano zina ufanano unaokaribiana sana. Uhusiano huu unahusishwa na kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na mawasiliano baina ya jamii moja hadi nyingine. Katika utafiti wao wanamsambao wamegawanywa katika shule mbili, kwanza ni kundi la shule ya India, kundi hili lilianzishwa na Jacob na Wilhelm ambapo walikusanya hadithi mbalimbali huko ujerumani na kwingineko barani Ulaya na kugundua kuwa ngano hizo zilikuwa na uhusiano na kuhitimisha kuwa ngano za Ulaya kama zilivyo lugha za Ulaya zimeonekana na rangi ya nasaba bora iliyopata kuishi huko kati ya kaskazini na Asia, rangi ya nasaba bora si rangi ya ngozi bali ni familia ya lugha ambayo lugha zote za Ulaya zinahusishwa nayo. Hivyo aligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa na makundi ya wahamiaji. Wao waliona chimbuko la ngano ni huko India na zikafika huko Magharibi kwa njia ya msambao.
Kundi la pili ni kundi la shule ya Kifini, shule hii ilianzishwa na Eliasi Lonnrot ambaye mwaka 1825 alianza kukusanya ngano za mashujaa katika nchi ya Finland, kupitia maudhui yanayohusiana na kuziweka katika kundi moja.
Ubora wa nadharia hii, wanamsambao waliipa hadhi fasihi simulizi kwa kuchunguza muktadha kwa undani, vilevile, nadharia hii ilionekana kuwa ni ya kisayansi zaidi, hivyo inaweza kuchunguzika tofauti na wanamabadiliko kwani akili ya mtu haiwezi kuchunguzika.
Upungufu wa wa nadharia hii, kufikiria kuwa ngano zimeenea toka kundi moja la watu hadi kundi jingine, inaonesha kuwa jamii ya Kiafrika haikuwa na ngano. Nadharia hii inaona kuwa Afrika haikuwa na ngano kwani ngano zilitoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) jambo ambalo si kweli kwani hata kabla ya ujio wa wakoloni Waafrika walikuwa na ngano zao. Vilevile, licha ya kuipa fasihi simulizi upekee katika kipengele cha muktadha lakini hawakuchunguza kwa undani vipengele vya kisanaa vya fasihi simulizi, mfano hawakuangalia vipengele muhimu vya fasihi simulizi ya Kiafrika hususani sanaa ya jadi kama vile, miviga, jando na unyago, matambiko, n.k.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, ukiangalia kwa jicho la ndani nadharia hii inasaidia kutambua kuwa mfanano wa ngano katika jamii nyingi za kiafrika ulitokana na maingiliano ya shughuli za kijamii kama vile, biashara, kilimo,ufugaji, uwindaji na kazi mbalimbali za jamii.
Nadharia ya umuundo, nadharia hii iliasisiwa na Claude Levis Strauses, alidai kuwa utamaduni unajumuisha vitu mbalimbali vinavyofanana, alichunguza visasili na kusema kuwa visasili hivyo vinatumika katika kuelezea na kutatua matatizo katika jamii. Hadithi hizo zilikuwa zinaelezea falsafa ya jamii husika, alidai kuwa visasili hivyo vilisaidia jamii katika kuyaelewa na kutatua matatizo ambayo yalileta mtanziko katika maisha ya binadamu, matatizo hayo ni kama vile, uhai na kifo.
Strauses, alidai kuwa muhusika wa ngano anajengwa katika kupambana na tatiziko ambalo anashindwa kulipatia majibu. Dominique Zahen aliongeza kuwa ngano zinahusu uhai na kifo na ziishie kwa kuona kuwa uhai na kifo vimetoka kwa mungu (mfano: ngano inayoelezea namna kifo kilivyoingia duniani) (rejea Miruka 1994:138)
Ngano zinatakiwa kutazamwa kama mfumo wenye kanuni zake ambazo kila msanii anatakiwa kuelewa pia aelewe mfumo unavyoweza kutumiwa katika mawasiliano na hata kimuundo. Mfano katika ngano lazima kuangalia matumizi ya lugha na kaida zinazotawala utunzi huo.
Ubora wa nadharia hii, nadharia hii inasisitiza kuwepo kwa kanuni/kaida maalumu za kiutambaji, kiutunzi na matumizi ya lugha. Hapa wanaona kuwa ngano zisichukuliwe kama kitu pekepeke bali ni utanzu unaoongozwa na kaida maalumu katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha. Hivyo kutakuwa na sifa zinazofanana katika ngano zote. Vilevile, inasaidia kujua chimbuko la ngano katika jamii fulani.
Udhaifu wa nadharia hii, kwanza kwa kutumia nadharia hii hatuwezi kupata kanuni rasmi ya kiutambaji, kiutunzi na matumizi ya lugha toka jamii moja hadi nyingine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila jamii ina namna yake ya kuwasilisha ngano zao, kuziumba ngano zao na matumizi ya tofauti ya lugha. Mfano; maumbo ya ngano yanatofautiana toka jamii moja hadi nyingine, mfano, muingiliano wa tanzu moja katika nyingine, utambaji pia hutofautiana, mfano watambaji na tabaka tawala na watambaji na tabaka duni. Hata wahusika wa ngano pia hutofautina mhusika anaweza kuwa mtu duni kwenda bora au mtu bora kuwa mtu duni. Nadharia hii pia inatalia mkazo muundo kuliko dhima ya ngano katika jamii.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadhairia inasaidia wanafasihi kutambua/kuelewa ngano kama utanzu wa fasihi una muundo wake rasmi katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha kiulemwengu lakini muundo huo si wa kimajumui kwa maana huweza kutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
Nadharia ya urasimi, nadharia hii iliasisiwa na mwanazuoni wa Kinesi Vladimir Propp (1928,1968) katika chake cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vema kuanza kuchunguza aina za ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika.
Ubora wa nadhairia hii, nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s)
Udhaifu wa nadharia, nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na wahusika wasiowaelevu/wajinga mfano fisi.
Nadharia ya saiko-changanuzi, muasisi wa Nadharia hii ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu alikuwa tabibu wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia, alichunguza hasa sehemu ya nafsi iliyofichika yaani sehemu ya ung’amuzi bwete ili kujua asili ya tatizo la mgonjwa husika, alieleza kuwa ung’amuzi bwete ni sehemu ya akili ya binadamu ambayo huhodhi fikra, mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo haiwezi kukubalika na jamii. Hofu na mawazo hayo hujitokeza kwa ndoto. Pia ung’amuzi bwete huhusisha matukio yaliyotendeka zamani lakini mgonjwa huyaingiza katika maongezi yake kama yanatendeka muda huo. Kutokana na utafiti wake aligundua kwamba ndoto zote husheheni ukweli kuhusu maisha ya mgonjwa.
Freud anaifananisha kazi ya fasihi na ndoto kwa kuwa visasili huwa ni hadithi za kubuni basi ubunifu huo unashabihi ndoto kwani wahusika wake na maudhui yake kwa ujumla huwa katika ulimwengu wa kufikirika ambao ni kama ndoto katika ulimwengu halisi sawa sawa na mgonjwa wa akili anayeumba ulimwengu wake.
Freud alisisitiza mambo yote katika akili ya binadamu yanatawaliwa na ngono (libido). Mawazo yake yaliungwa mkono na mwanafunzi wake Carl Gustav Jung ambaye pia alifanya kazi pamoja na Freud katika kuwatibu wagonjwa wa akili kwa kutafsiri ndoto ingawa Gustav alitofautiana na Freud kwa msimamo wake kuwa akili ya binadamu inatawaliwa na ngono.
Carl Gustav Jung alifanya utafiti na kuunda dhana ya kikale ambayo ni mtiririko au picha kongwe inayojitokeza mara kwa mara katika tajriba anayopitia mwanadamu , alisema kuna sehemu ndani ya akili isiyokuwa na fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa juu ya mawazo na matendo yake. Alitofautisha sehemu hiyo kama, sehemu ya kwanza ni sehemu binafsi inayofunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake na sehemu ya pili ni sehemu ya kijamii inayofunza maarifa ya kibinadamu yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa kwa karne nyingi. Anasema sehemu hii husika na matambiko muhimu ambayo mtu anapitia kama sherehe za kumpa mtu jina, sherehe za kuingia jandoni na unyagoni, sherehe zinazoigizwa wakati wa ndoa na hatimaye sherehe zinazohusu maziko ambazo sherehe zote hii ndizo huibua ngano.
Gustav alifafanua kwa undani masuala ya ngano katika tamaduni mbalimbali za dunia. Hivyo Freud na Gustav wanasema masimulizi ni kama ndoto au mvurugiko wa akili kwani picha, taswira na maudhui vyote ni vya kubuni havitoki katika ulimwengu halisi.
Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii inaonesha utofauti wa msimulizi mmoja hadi mwingine hutokana na historia ya mtu binafsi na uwezo wake binafsi hata kama kisa kitakachosimuliwa ni kimoja, hii imedhihirishwa kwa wagonjwa waliokuwa wanasimulia mambo yao kwa utofauti kutokana na historia zao. Lakini pia imesaidia kutuonesha chimbuko la ngano kwa miktadha tofauti tofauti kama sherehe za jando na unyago, sherehe za kutoa jina, n.k.
Upungufu wa Nadharia hii, Nadharia hii imesisitiza zaidi masuala ya hisia za kingono katika ubunifu wa masimulizi kitu ambacho hakina ushahidi wa kutosha kwani siyo kila hadithi inatarajia kujiridhisha kutoka hali ya ngono iliyofifizwa katika ung’amuzi bwete kama anavyosema Freud.
Nadharia ya kiuamilifu, Nadharia hii iliasisiwa karne ya 20 na Poland Bronislav Malinowsk. Uamilifu uliibuka kama njia yal kuyatazama maisha na utamaduni wa jamii, kwa kuchunguza dhima za vipengele vya kijamii pamoja na njia ambazo kwazo dhima hizi zinahakikisha uwepo wa jamii. Malinowsk alifanya utafiti Australia na kugundua kuwa ngano ni kumbukumbu za kweli za mila na desturi za jamii zilizopita, unyago, jando, mazishi, harusi, tohara, matambiko, kusalia miungu, n.k.
Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii imesaidia kuondoa mawazo kuwa chimbuko la fasihi mbalimbali zikiwemo ngano ni mahali fulani bali ni kila jamii imekuwa na simulizi ambazo zinasawiri tajriba (uzoefu) wao wa kila siku katika Nyanja mbalimbali kama vile, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Vilevile Nadharia hii, inatusaidia kujielewa na kuzielewa jamii zetu vizuri, kwa kuyaelewa mazingira ya mila na desturi zetu katika jimii.
Nafasi ya Nadharia hii katika ngano za Kiswahili, inatusaidia kujua tamaduni zetu katika somo la ngano, pia inatusaidia kujua kuwa kila jamii ilikuwa na tamaduni zao zenye kuwaongoza katika maisha yao ya kila siku kama vile, jando na unyago, harusi, matambiko, mazishi, miviga, kusalia miungu kuwa ndiyo chimbuko la ngano.
Hitimisho, kila nadharia tuliyoiangalia ina umuhimu wake katika kujifunza chimbuko la ngano, hivyo ni muhimu kila mwanataaluma wa ngano kuzisoma na kuzielewa nadharia zote zinazozungumzia chimbuko la ngano kwa sababu kila nadharia ina misingi yake ambayo kwa namna moja ama nyingine inatusaidia kujua na kuelewa chimbuko la ngano, Nadharia hizi ni muhimu pia kujifunza kwa sababu kuanzishwa kwa nadharia inategemea na upungufu unaojitokeza katika nadharia nyingine. Kwa ujumla licha ya mtenguo wa nadharia moja dhidi ya nyingine tunaona kuwa Nadharia hizi zinakamilisha, Nadharia moja inakamilisha Nadharia nyingine. Kwa maana hiyo, hatuwezi kujua au kuthibitisha chimbuka la ngano kwa kutumia nadharia moja.