B. F. KIWALE
P.O BOX 774
IRINGA
© Kiwale, F. Brasto 2016
ISBN 9976 911 59 1
chapa ya PILI 2016, January 2016.
Haki zote zimehifadhiwa. hakuna sehemu ya kazi hii itakayo ruhusiwa kuirudia kuitengeneza, kwa namna yoyote ile, bila ruhusa ya mwandishi au B. F Consult P.O. Box 774, IRINGA.
Printing and publishing consultancy by
KIWALE org/ TFC, P.O Box 327,
Iringa, Tanzania.
Ushairi
ni sanaa ya lugha inayoeleza jambo au wazo kwa njia ya mkato, na kwa namna
inayoleta hisia za msomaji au msikilizaji.
Maneno ya mashairi huteuliwa kimakusudi (ili yalete taswira maalum
akilini mwa msikilizaji au msomaji).
Maneno hayo pia hupangwa ili yatoe mdundo fulani shairi linapoimbwa,
linaposomwa au linapoghanwa (Njogu, 1999:87).
Kwa
ujumla, ushairi ni sanaa ya lugha inayotumia lugha ya mkato, maneno ya hekima,
lugha ya picha yenye mpangilio fulani wa vina na mizani unaovuta hisia za msomaji
au msikilizaji ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa.
Muktadha wa utanzu
wa ushairi wa kiswahili katika kipengele cha fani umekuwa ukitumiwa na vipindi
vyote viwili yaani kipindi cha zama hizi na kipindi cha ushairi wa zilipendwa,
kwa namna tofautitofauti kupitia vipengele vifuatavyo;
Matumizi
ya lugha, katika muktadha wa utanzu wa ushairi wa kiswahili wa zama hizi; lugha
inayotumika ni rahisi na inayoeleweka kwa hadhira, kwa kuwa washairi wa sasa
hawafungwi na kanuni za ushairi wa kijadi. Kwa mfano, msanii Roma katika wimbo
wake wa “Mathematics” anasema
“…Nchi imeuzwa vigogo wanatuita ATM
Tuwakemee
mafisadi wote wa CCM…”
Hivyo kupitia
kipande hiki hadhira inapata ujumbe wa moja kwa moja wa ufisadi. Lakini ushairi katika zama za zilipendwa
lugha iliyokuwa inatumika ni ngumu kutokana na uthibiti wa tabaka tawala. Pia
uzuri wa ushairi wa kipindi hicho ulibainishwa kupitia lugha nzito, mfano
Shaaban Robert katika shairi la “Mtu na Malaika” anasema “…Wa huku hafiki huko, wala halina
malisho,
halishibishi kuchosha,
njiaye ina uchovu,
na tabu inayokwisha, wala
hupati utuvu… (Mlokozi, 1979:30).
Taswira,
katika zama hizi taswira zinatumika hususani katika suala la mapenzi kwa lengo
la kupendezesha kazi zao. Mfano Msanii
Ngwea katika wimbo wake wa “Kimya kimya” anasema; “…watu wanazamia hadi uchumvini…” akimaanisha watu wa
kileo wanafanya tendo la ndoa bila umakini.
Pia katika uchumi ushairi wa zama hizi umekuwa ukitumia taswira kwa
lengo la kuelimisha jamii mfano msanii Solo Thang katika wimbo wake wa “Miss
Tanzania” anasema “…Maliasili
ndo kitasa kila funguo, inapita…” Akimaanisha uwekezaji wa masharti
nafuu. Katika zama za kale/au mashairi ya zilipendwa yalitumia ujenzi wa
taswira kwa kurejelea vitu au mambo yaliyopendwa zaidi zama hizo, mfano wimbo wa Miriam makeba wa “malaika” ulitumika kujenga
taswira juu ya matendo ya mwanamke mwema kwa mumewe “...sina
neno mimi, kwa kuwa najua, penzi upepo
penzi maam… ipi siku…, penzi upepo, penzi
maua…”
msanii huyu anajenga taswira ya namna penzi
linavyoweza kunawili au kudhoofu kutokana
na linavyotunzwa kama ua liweze kunyauka au kustawi kutegemeana na
matunzo unayoyapata.
Muktadha wa
utanzu wa ushairi wa Kiswahili katika zama hizi na zilipendwa maudhui
yamejibainisha kwa namna tofautitofauti kupitia dhamira zifuatazo;
Suala
la utawala na uongozi, wasanii wa kipindi hiki wengi wao wamekuwa wakiwakosoa
moja kwa moja viongozi wanaoenda kinyume na taratibu za uongozi. Mfano Msanii
“Ney wa Mitego” katika wimbo wake wa “Salamu zao” anasema “…Ridhiwani mwambie dingi yako masela
hatumuelewi” Pia Roma katika wimbo wake wa “Mathematics” anasema ‘‘…mauti yangetufika bila kumpiga
Jakaya…” washairi wa kimapokeo waliandika wasifu wa viongozi wa zama
hizo, mfano, Katika utenzi wa “Fumo Lyongo” alitunga shairi la kumsifu mfalme, (Uk 13 ubet 13). “…Ni mwanamume Swahihi, kama simba una zihi...” Pia
Ottu Jaz Band wimbo wa “Naye Mwalimu Nyerere”(1970) wanasema “Naye mwalimu Nyerere jemedari wa
Afrika”
Suala
la mapenzi washairi wengi wa zama hizi wanazungumzia suala la mapenzi kwa kiasi
kikubwa zaidi ya asilimia 50 wanazungumzia mapenzi kwa sababu mapenzi yana soko
kubwa. Mfano Msanii Zay-B katika wimbo
wake wa “Ananitesa” anasema
“…Nakupenda
pia nakutaka pia..” Pia msanii K-Lynn na Bushoke katika wimbo wa “Machozi
ya fuaraha” wanasema “Mapenzi si
maneno, mapenzi ni vitendo”
pia katika zama za zilipendwa washairi
walizungumzia suala la mapenzi ili kuelimisha tu jamii lakini si kwa ajili ya
soko tu. Mfano katika utenzi wa Mwanakupona (Uk 112) ubeti 47 msanii anasema
“…ukae na mume wako…”
Suala
la utamaduni, washairi wa zama hizi baadhi yao hutweza utamatuni wao na
kuukweza utamaduni wa kigeni, mfano, Vanesa Mdee katika wimbo wake “Come over”
anasema “…Uliniomba namba nami
nikakataa! Oooh! I think about you baby” (Nakuwaza sana mpenzi). Hivyo
wapo baadhi wanaousifu utamaduni wao. Mfano.
Mr. Ebbo katika wimbo wa “Mimi Mmasai” uliopo katika albamu ya “Fahari yako”
anasema;
“…Mimi Mmasai bwana
nasema mimi Mmasai, tamaduni yenye nguvu iliyobaki Afrika…” Katika swala
la utamaduni wakati wa zama za zilizopendwa washairi walitunga kazi zao kwa
kutumia lugha zao kuusifu utamaduni wao. Mfano Shaaban Robert katika shairi la
“Titi la Mama” anasema;
“…Kiswahili
naazimu, sifayo iliyofumbwa…”
Pia katika
kipengele cha ujumbe katika ushairi wa zama hizi hutolewa katika kali ya uwazi
bila kificho mfano katika kitabu cha “Uzalendo” shairi la “Kweli iko wapi”? (uk.37) Msanii anasema
“…Cheche
ulipozitema, orodha ukisema,
mchafu asosafika, vipi lulu
kageuka?
Mshairi anamaanisha kuwa viongozi
wengi ni wanafiki katika kutoa maamuzi mfano, wapo tayari kuwapokea waovu kwa
maslahi binafsi. Katika zama za zilipendwa aghalabu ujumbe ulitolewa kwa uficho
huku mshairi akifikirisha zaidi hadhira, kwa sababu uzuri wa ushairi wa kipindi
hicho ulibainishwa kupitia lugha nzito.
Mfano Shaaban Robert katika shairi la Mtu na Malaika anasema “…wa
huku hafiki huko wala halina malisho…”
Hivyo basi, Kuna utofauti wa
muktadha wa ushairi wa Kiswahili wa kisasa na ule wa zama za zilipendwa, kwani
muktadha wa zilipendwa ulifungwa na sheia za vina na mizani, kwa sasa muktadha
wa ushairi wa sasa upo huru (hakuna sheria zinazombana) jambo lililopelekea
wasanii kuwa wengi kaibuka.
No comments:
Post a Comment