Friday, 24 July 2015

FALSAFA YA KIAFRIKA NA RIWAYA YA KISWAHILI

John mbiti
Huyu ni mwanafalsafa maarufu aliyezaliwa nchini Kenya, alitumikia waasifu wa uparoko katika kanisa la Roman Catholic (RC). Aliandika maandiko mawili yaliyotalii falsafa ya kiafrika “Africa Religious Philosophy (1966) and African concept of God (1970). Alizungumzia yafuatayo kuhusu falsafa ya kiafrika.
Dhana ya wakati; kwa waafrika hawaangalii wakati na hawana haraka na wakati, mwafrika katika kuangalia wakati, namba za saa ni kitu dhahania, kwa mwafrika wakati hauamui matendo kama ilivyo kwa mzungu, dhana hii imedhihirika katika riwaya ya “ Nagona” kwa muhusika babu alipokuwa akimweleza mjukuu mwaka wake wa kuzaliwa kwa kuyarejea matukio kama matukio ya “utupu” ajali gharika kupatwa kwa jua kama asemavyo mwandishi.
“……nataka kujua habari za kuzaliwa kwangu wazazi wangu hajapata kunieleza kikamilifu….. natakueleza. Hivi ndivyo ilivyokuwa…….hapakuwa na ujuzi wa jema na baya. Hapakuwa na fikra. Palikuwa na utupu katika kitovu cha undani na hapakuwa na nguvu zilizoweza kutoa uongozi…….. ajali hii ilitokea katika bonde la hisia……. Katika ukweli huu palitokea gharika katika mto wa bonde…..(uk 11)”.
Vilevile katika kitabu cha riwaya ya “Mirathi ya hatari”  wazo limethibitishwa na familia ya Mzee Kazembe alivyokuwa akijilimisha usiku na mchana bila hata ya kuangalia wakati.      “……si yule wa mji wa Kazembe ajilimishaye usiku na mchana..(uk 5)”.
Hata katika mazingira halisi ya waafrika mambo haya yanahalisika.
Dhana ya kifo, Mwafrika anapokaribia kufa huwa anatoa urithi mfano mali, uchawi, jina au maelekezo fulani kuhusu baraka au laana katika “Mirathi ya hatari”, Gusto, kijana wa Mzee Kazembe aliachiwa urithi wa pesa, Mirathi ya hatari (uchawi), mashamba pamoja na baraka anasema.
“….mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukitumia vema; bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo. Nakuachia dawa zote na milki yangu katika mizungu ya sihiri…(uk 15-16)”.
vile vile, Dina alimuachia maagizo Gusto alisema
 “mali yangu yote isipokuwa kitabu kilicho sandukuni mwangu, uwape maskini” (uk 90).
Pia katika kitabu cha “Nagona” Babu anatoa maagizo au maelezo kwa mjukuu wake baada ya kukaribia kufa alisema
“…. Mjukuu jihadhari siku ya ngoma kuu usikanyagwe daima fuata duara na macho yako wakati wote watazame hapo katikati hicho kitovu kitakapo pasuka mengi yaliyofichika kwa karne nyingi yataonekana harafu kwa shida alisema Nag…..Nag….” (uk 45).
Dini, kwa mwafrika , dini ni chimbuko la mambo yote na kwa asili mwafrika alizaliwa na dini yake, si suala la kujifunza na kusilimishwa; katika “Mirathi ya hatari” ametumia familia ya Mzee  Kazembe, Madoda na Mavengi waliokuwa na dini yao ya asili ilivyokuwa ikifanyika mapangoni usiku pamoja na baadhi yao kuamini dini ya kujifunza na kusilimishwa lakini hawakuiacha kamwe, kama asemavyo mwandishi;
                        “enyi mahoka wa mababu;
                                Enyi wazee mliotangulia
                                Enyi wenzangu,
                                Sikiliza kiapo changu!
                                Sitasema wala kuwaza lolote,
                                La ndani ni la ndani!
                                Nishindwe mara tatu,
                                Pembe hili linichome moto…!(uk 22)
Haya ni maneno yanayoonesha utii wa dini za asili zenye kuamini miungu, mahoka, wazee na binadamu.
Pia katika riwaya ya “Nagona” mwandishi amemtumia mhusika Padri ambaye alikuwa anaamini dini ya kujifunza na kubatizwa (Ukristo) na Wazee walishikiria dini ya kipagani kama dini ya asili kama asemavyo;
“…Padri alikaa kimya, wazee wote walimtazama, Padri alitabasamu aliwatazama wazee halafu akafungua kinywa chake, hakuna mkristo miongoni mwenu?” wazee walitazamana “ Hakuna” babu alijibu. (uk 10).

Hii inadhibitisha kuwa waafrika wanaozithamini dini zao za asili na kuzitupilia mbali dini za wageni kama ukristo hii hata katika mazingira halisi ya kiafrika imetawala sana hususani maeneo ya vijijini.
Kuhusu ufahamu wa ulimwengu na uwapo, waafrika wanaamini kuwa ulimwengu uliumbwa na Mungu na Mungu ndiye muumba wa vyote. Mfano katika riwaya ya “Nagona” imejidhihirisha katika majibizano ya Padri na Mtubu dhambi kama asemayo mwandishi;
                        “…Mmh! Baba unazo dhambi zingine”
                                “kubwa moja na ndogo nyingi”
                                 Lakini unajibebesha mzingo mzito! Dhambi za karne mbili!”
                                “Mungu aliumba ulimwengu na vyote vilivyomo…….” (uk 51)
Pia katika kitabu “Mirathi ya hatari” mwandishi amemtumia Gusto kama mhusika aliyekabiliwa na changamoto nyingi kutoka kwa wanafunzi wenzake katika safari yake ya masomo ila kwa kuwa alimwamini Mungu ndiyo chanzo cha yote hapa duniani alijipa moyo atayashinda kama asemavyo;
“…. Kwani yaliyopita si ndwele tugange yajayo kwa uwezo wa mbingu natumaini nitafanikiwa, sijui nianzie wapi” (uk 4).
Hivyo basi nukuu hii inaonesha jinsi waafrika wanavyotumaini Mungu kuwa hata mambo yawe magumu ama mepesi kuwa ndiyo yeye pekee anayeyajua kwani ndiye aliyeyafanya yawepo hapa dunia au ulimwenguni.
Kwa ujumla John Mbiti anaona kuwa falsafa ya kiafrika ipo na inaendelea kuwepo, na uwepo huo unajidhihirisha katika mambo ya kiutamaduni, japo athari za kiutamaduni wa kigeni unaokweza na sababu za maendeleo ya sayansi na teknolojia na zile za kiutandawazi.
Kwasi Wiredu
Ni miongoni mwa wanafalsafa wa kiafrika, alizaliwa mwaka 1931 katika nchi ya Ghana yeye aliangalia dhana ya Ngano na hadithi. Na jinsi gani zinavyojidhihirisha katika falsafa ya kiafrika. Kwasi Wiredu alidai kuwa waafrika hawana falsafa yao wenyewe bali mawazo yao hujiegemeza katika mapokeo ya watu wa magharibi. Hivyo Kwasi Wiredu katika kulinda mtazamo wake ametoa baadhi ya hoja madhubuti kuhusu kutokuwepo kwa falsafa ya kiafrika.
Hoja zake zinaweza kuwa na ukweli fulani na zisiwe na ukweli fulani kulingana na uchunguzi uliofanyika kwa kutumia riwaya ya “Nagona” na ile ya “Mirathi ya Hatari” kama ifuatavyo:
Mawazo ya kiafrika ya kiutamaduni na kijamii huwa hayabadiliki kulingana na wakati. Suala hili la kutobadilika kwa utamaduni sio tu kwa Afrika bali ni duniani kote. Hii hutokana na waafrika kushikilia baadhi ya misimamo yao kiutamaduni bila kujali mabadiliko ya wakati kutokan na waafrika wenyewe kutoruhusu fikra mpya. Haya yanadhirishwa kwenye riwaya ya “Nagona” japokuwa utamaduni unabadilika lakini mawazo ya kiafrika yanabaki vilevile. Mfano suala la ndoa katika riwaya hii mhusika Mimi alipotaka kumkumbatia msichana ambaye alilkuwa bado hajaolewa ilikuwa ni kinyume na tamaduni za kiafrika mwandishi anasema;
“….nilipomkaribia niliinua tena mikono yangu kuukumbatia mwanga. Lakini aliishika mikono akaishusha tena mahali pake akisema.
“Mila”  
“mila gani?”
Myeleka lazima kwanza tupige myeleka ukifanikiwa kunishika na kunitupa kitandani basi umeshinda. Sitakuwa na la kusema. Utaruhusiwa kucheza ngoma kati kati ya duara” (uk 67).
Hii inaonyesha kuwa pamoja na mabadiliko ya wakati lakini bado waafrika wana mawazo yao juu ya utamaduni kwani hata katika jamii zetu mawazo kama haya bado yapo. Mfano, wamasai na wasukuma ili uweze kuoa binti wa kimasai lazima ufuate utamaduni. Pia katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mtunzi anaonyesha hayo pale mtunzi anaposema;
majira ya wakati yanabadilika mzee wangu…..ukweli ni kwamba sisi wenyewe wazee ni wa kulaumiwa tumeshindwa kutambua kuwa dunia ya leo si dunia yetu….tumeshindwa kutambua kwamba ulimwengu wa leo ni ulimwengu unaobadilika kwa kasi tusiyoweza kuimudu…. Nani kati yenu angetegemea kufika hospitalini na kupimwa huku na mwanamke mwafrika ambaye pia huendesha gari lake mwenyewe (uk 56)”

Hii inaonyesha dhahiri kuwa mawazo ya waafrika hayabadiliki kwani wazee wanashangaa jinsi wanawake wanavyoweza kufanya kazi ambazo hapo awali zilikuwa zikifanywa na wanaume katika jamii zetu pia tuanona kuna wazee ambao bado wanalalamika kwa jinsi waonavyo ulimwengu ulivyobadilika. Kwani kuna mawaziri, wabunge na wakuu wa mikoa.
Afrika hakukuwa na falsafa kwa kuwa mawazo yao yanahusisha wahenga na haina uthibitisho tofauti na ile ya kimagharibi. Kwasi anaamini kuwa Afrika hakuna falsafa kwa kuwa haikuandikwa bali mawazo yao yalihusisha Wahenga tu. Haya yanadhirika kwa kutumia riwaya ya “Nagona” pale mtunzi anaposema;
“…sauti ya kiwiliwili ilisikika kutoka katika mwanga, kwa sasa mazungumzo na roho yako yanatosha utakapo jua kuzungumza na roho yako vizuri mambo yataenda kwa haraka kidogo…..huu si mwanzo mbaya meza roho  yako….”(sura ya tatu (3).
Hii inaonyesha kuwa waafrika wakipata matatizo hukimbilia kuwaomba wahenga ili waweze kuwasaidia katika matatizo hayo. Katika jamii yetu pia kukiwa na matatizo wazee wa jamii huenda kuzungumza na wahenga ili waweze kuwasaidia, mfano katika jamii ya Wangindo wakipata  matatizo huenda “Ngende”. Pia katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kuna mawazo yanayohusishwa na wahenga pale watu wapatapo matatizo;
                        “enyi mahoka wa mababu;
                                Enyi wazee mliotangulia
                                Enyi wenzangu,
                                Sikiliza kiapo changu!
                                Sitasema wala kuwaza lolote,
                                La ndani ni la ndani!
                                Nishindwe mara tatu,
                                Pembe hili linichome moto…!(uk 22)
Lakini kutokana na Kwasi anadai kuwa mawazo hayo ya Wahenga hayawezi kuthibitishwa kwa sababu hayakuweza kuandikwa katika andiko lolote bali yalikuwa ya kurithishwa tu. Hivyo hakuna falsafa ya Kiafrika.
Kinachoitwa falsafa ya Kiafrika kinajumuisha hekima, elimu, mila na desturi ambapo kwa Kwasi Wiredu anasema; vitu hivi haviitwi falsafa lakini matendo au vitu hivyo vyote vilikuwa vikifanywa na waafrika, kwani vinajidhihirisha kama ifuatavyo; Kuhusu hekima, huangalia matendo mema na maneno ya busara yaliyokuwa yakifanywa na waafrika hasa wazee wa zamani na hivyo huweza kurithisha hekima hizi kwa vijana au vizazi vya sasa. Katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” Mzee Mavengi alimshangaa Gusto alivyokuwa akitoa maneno ya hekima kwa wenzie kuliko vile alivyokuwa akidhania.
            “…hivyo nadhani kuna chembe fulani ya ukweli na hekima fulani katika maneno yako…” (uk 26- 27)
Hii ni dhahiri kuwa Gusto alikuwa kijana mwenye hekima ambaye ni moja kati ya viashiria vya mawazo ya kifalsafa.
Kuhusu elimu, huangalia elimu ya awali kwa waafrika ambayo ni jando na unyago ambayo humuandaa kijana katika kupambana na mazingira yake na jamii kwa ujumla katika kudhihirisha hili katika riwaya ya “Nagona” mwandishi nanaonyesha kuwa waafrika walikuwa na njia/ chombo chao cha kutolea elimu ambacho ni jando;
            “….hatutaki ajali nyingine. Bado hujaenda jandoni, ukivalishwa ushanga…”(uk 20)
Elimu hii pia bado inatolewa katika jamii tafautitofauti za kiafrika mfano kimakonde.
Kuhusu mila na desturi, waafrika wanamila na desturi zao kama vile namna ya kusalimia, maisha yao na kurithisha mali ni desturi ya waafrika. Mawazo haya ambayo yalisemwa na Kwasi Wiredu yanadhihirishwa katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” .
            “….mwanangu nakuachia kazi kubwa, ni urithi mkubwa ukiutumia vema…..” (uk 15)
Hapa baba Gusto anamrithisha mwanae mirathi ya hatari kama desturi ya waafrika wengi pale mzazi anapokaribia kuaga dunia anaendelea kusema;
            “….nakuachia dawa zote na milki yangu katika mizungu na sihiri…(uk 16).
Hayo pia yanadhihilishwa katika riwaya ya “Nagona” ambayo wazazi wanadesturi ya kuachia urithi wanao. Mfano, babu alipokuwa anakaribia kufa lakini mimi nimeacha mali gani nyuma? Hakuna isiyopokuwa wewe, baba yako na mama yako. Hii inaonyesha hata kama mzazi hana mali basi hupenda hata kuacha wosia kwa wale wanaobaki.
Mawazo mengi na tamaduni za kiafrika ni za kishenzi, ushirikina, uchawi na kupitwa na wakati. Hata wasomi wa kiafrika wanaamini mawe, mizimwi, miti, mapepo, mahoka na Miungu Kwasi anadai, kuwa hata kama mwafrika akisoma lazima atakuwa na tamaduni za kishenzi, kichawi na kushirikina hayo yanadhihilishwa katika riwaya kama zifuatavyo;  kuhusu uchawi, mwandishi wa riwaya ya “Mirathi ya Hatari” imejishughulisha sana na suala hili la uchawi kuwa mawazo waliyonayo waafrika kwa kiasi kikubwa. Gusto kijana mdogo tu wa shule alirithishwa tunguli (uchawi) na baba yake baada ya baba yake kufa, waafrika wengi huamini mazingaombwe kwa kila kitu hayo yanaonekana pale baba Gusto anasema;
          “….ukipatwa na adha
                Sihiri hii ikutulize
                Ukiona na hasidi
                Fingo hii impumbaze
utende mambo kwa idhaa
Kago hii ikuongoze…” (uk 23)
Pia katika riwaya ya “Nagona” mawazo ya kiafrika yamejikita katika suala hili la uchawikwa mfano anaposema;
            “….ndege wa mawio walipoanza kuwaimbia wachawi….(uk 23).
 Inaonesha waafrika huamini kiasi cha kushindwa kulala; “….hata wachawi hubisha  hodi…(uk 16).
 Hii inajidhihirisha kuwa mawazo ya waafrika yapo kwenye utamaduni wa kichawi. Pia kuhusu ushirikina, mwandishi anajaribu kuonyesha imani ya kishirikina kwa jamii za kiafrika, katika riwaya ya “Nagona” yanadhihishwa hayo kama ifuatavyo;
            “…na huyo paka! Yeye ndiye mlinzi wa kifo..(uk 9)”,
Wanajamii hii huamini kuwa paka anaweza kuwalinda dhidi ya kifo. Pia katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” Mzee malipula na wenzake wanajadili juu ya suala la safari ya kwenda Malawi kumpeleka Gusto wakajue nani aliyehusika na kifo cha Mzee kapedzile;
“…njia iliyobora ni kwenda Malawi kwa Chikanga yeye amejaaliwa na kipawa cha kujua yupi mcahwi yupi si mchawi…nilichanjwa kifuani nilichanjwa magotini na usoni na vidoleni chale zilipotoka damu nikapakazwa madawa ya aina aina….(uk 59).
Pia anaendelea kusema juu ya imani ya kishirikina;
 “…nilivishwa kitu kama hirizi…(uk 23)
hii imekuwa imani ya waafrika wakiamini kuwa hirizi inaweza kuwalinda dhidi ya magonjwa au wachawi. Hivyo Wiredu anashauri kuwa waafrika hawana budi kuachana na Mila hizi pamoja na imani hizi ambazo kwa sasa hazina nafasi tena.
Waafrika wanaamini uchawi miungu, uhalali wa utumwa na ukandamizaji wa mwanamke Kwasi Wiredu anashauri waafrika waachane na mambo hayo kwani hayana tija kwa maisha yao. Kuhusu Miungu, waafrika huamini katika miungu wanapopatwa na shida, shida hizo zilitatuliwa kutokana na imani hiyo ya Miungu. Haya yanadhihilishwa katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari”
“…shida ya mvua, homa, ukame na mengineyo mengi…. Mahoka ya mababu, …enyi wazee mliotangulia.., …pembe hili linichome moto…”(uk 22)
Pia katika Miungu wanasema
 “….Mahoka wamempokea vyema kwao…(uk 52)”.
Hii inaonyesha kuwa Miungu wamepokea maombi yao. Vilevile katika riwaya ya “Nagona” kuna Padri aliyekuwa akihubiri habari za Kristo.
“..mimi nahubiri habari za kristo wewe unahubiri upagani…”(uk 19).
Hii ni kwamba waafrika walikuwa wakiamini kwenye upagani. Hali kadharika kuhusu uhalali wa utumwa hupenda kutumikiwa utemi, kuwa juu ya wengine yaani kunyenyekewa na watu wa chini yao. Mfano katika “Mirathi ya Hatari”, Mzee mavengi, Mzee malipula na wengine  walikuwa ni watu wenye mamlaka katika kijiji chao. Mzee malipula alikuwa Balozi wa nyumba kumi alitumia madaraka yake kuwanyanyasa wengine;
            “…hivi unafahamu kuwa mimi ni Balozi wa nyumba kumi kumi hapa…” (uk 60).
Kuhusu ukandamizaji wa mwanamke, waafrika wengi waamini kuwa mwanamke si chochote ni mtu asiye na umuhimu mkubwa sana kuliko mwanaume katika jamii. Hapa ndipo mfumo dume hujidhihilisha, falsafa hii inapendelea mwanamke kunyimwa uhuru hasa katika elimu, kuchagua mume ampendae. Mfano katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” pale msanii anapobainisha haya yafuatavyo;
            “…kumsomesha mtoto wa kike ni kama kumpa bangi imvuruge akili….?(uk 56)
Inaonekana kuwa wanawake wa kiafrika hawaaminiki kabisa katika kufanya lolote huu ni mfumo dume kuonekana kuwa mwanaume ndiye kila kitu. Hivyo Wiredu anashauri kuwa waafrika hawana budi kuachana na fikra hizo kwani ni potofu badala ya kuendeleza kuwalinda kwa madai kuwa ni falsafa yao.
Kwasi Wiredu anaonekana kuamini sana falsafa ya kimagharibi na kupuuza falsafa ya kiafrika, lakini katika mitazamo yake inazua maswali yafuatayo; je ni kweli hakuna falsafa ya kiafrika? Kama haipo kuna nini? Kama ipo ipoje? Je uchawi na ushirikina ni falsafa ya kiafrika? Kama ndio kwa nini? Kwa vipi? Na kama sio kwa nini? Hivyo hayo ni maswali kadhaa ambayo amewaacha wasomaji wakiwa bado wanajiuliza na kutokupata jibu kwani hajaweka wazi mambo hayo yote.
Placide, J.W. Temples
Huyu pia ni mwanafalsafa ambaye alikuwa padri aliyeishi nchini Kongo mwenye asili ya ufaransa na aliishi 1906 hadi 1977 alifanya uchunguzi juu ya sayansi ya makabila. Hivyo aliangalia falsafa ya kiafrika na kutoa baadhi ya mambo aliyoyachunguza kama ifuatavyo;
Maisha na kifo, mwanadamu katika fikra zake zimetawaliwa na vitu viwili yaani uhai na kifo, hivyo kwa waafrika mtu anayeweza kupunguza maisha ni mchawi na anayeweza kuongeza maisha ya mwanadamu ni mganga, hivyo waafrika wakipata matatizo huzirudia imani zao za jadi na Wahenga au mizimu huachiwa suluhisho la matatizo na wahenga wananguvu kuliko waliohai na hakuna kifo kisicho na sababu na kinatokana na uchawi. Hivyo haya yote yanajidhihilisha katika Riwaya ya “Mirathi ya Hatari” hivyo mwanafasihi anasema;
            “.. waaidha nilipewa kisu nikaonyeshwa sehemu za kukata…..”(uk 43)
Kutokana na kifo cha Mzee kapedzile sababu zilitolewa na Mzee malipula na Mzee mavengi kuwa aliyehusika ni Gusto.
“…..unasemaje nini, Dina? Mlifanya nini jana usiku?” ..usinidanganye sasa Gusto nafahamu yote, jana mmekutana na wale wazee mkamuua Kapedzile…..(uk 51).
Ukweli ni kwamba hata katika jamii zetu yapo mfano katika kabila la wabena kama mtu amefariki kwa ajali, au kufa ghafla ama kwa homa bado huwa inasadikika kuwa anaweza akawa ameuawa na miongoni mwa ndugu zake ili wapate kufanikiwa, na hii haipo katika jamii ya kusini tu mwa Tanzani bali ni viwakilishi tu kwamba jamii yote ya kiafrika mambo haya yapo.
Dhana ya kuhusu Mungu, Mwafrika anaamini kwamba kuna ngazi tofauti tofauti za kumfikia Mungu mkuu ambaye ndiyo nguvu kuu, Mizimu, Wahenga (walio kufa), Wazee waliohai, binadamu (mtu wa kawaida). Hivyo dhana hii inajidhihirisha katika riwaya ya “Nagona” ambapo mizimu imeonyeshwa kupitia Jogoo ambaye ni mzimu wa kulinda kisima, Paka Mzimu wa kulinda nyumba na kisima hicho cha damu. Pia Wahenga wazee waliokuwa wawili waliobakia pale kijijini walikuwa na uwezo wa kuwasiliana na mizimu, ambapo mizimu hiyo hufikisha taarifa kwa Mungu Mkuu. Kwa mfano Mzee aliyekuwa akilinda kisimani pale alikuwa anapata taarifa kupitia kuongezeka kwa damu kuwa kuna mtu atakuja.
Pia dhana hii ya imejidhihirisha katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” ambapo Gusto alikuwa na nguvu za sihiri bado aliamini kuwa Mungu bado yupo alichukuliwa na Madoda kwa ajili ya kuapishwa kuwa ndiye mrithi wa cheo kile alichokuwa nacho baba yake, lakini baada ya kuamka siku ya jumapili bado alijiandaa kwa kwenda kanisani, mfano;
“….niliporudi niliingia chumbani nikavaa nguo zangu rasmi tayari kwa kwenda kanisani… (uk 29).
Hivyo hii inaonesha jinsi waafrika wanavyoamini Mungu kuwa hata mambo yawe magumu au mepesi kuwa yeye pekee anayeweza kuwafanikishia mambo yao. Japokuwa waafrika tangia awali tulikuwa na dini zetu.
Mwafrika anaamini kuwa kuna watu wenye nguvu ya kubariki na kutoa laana pamoja na viongozi au wazee au watu mashuhuri. Hivyo wazo hili ni mojawapo ya mawazo ya Temples amejaribu kuwaainisha waafrika na kuona kuwa waafrika wanaamini hivyo katika maisha yao hasa pale mtu anapokuwa anaishi ama anakaribia kufa. Hivyo basi wazo hili linajitokeza katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mwandishi amemtumia Mzee kazembe alimwita Gusto ili ambariki ampe mirathi. Lakini vilevile Mzee kazembe hakutaka kusogeleana na Rafael aliyekuwa amejitenga na kupewa laana na wazazi wake.
“….mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukitumia vema; bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo. Nakuachia dawa zote na milki yangu katika mizungu ya sihiri …(uk 15)”.
Pia Mzee malipula alimlaani binti yake Dina kuwa hawezi kufanikiwa baada ya kuonekana anataka kuolewa na Gusto ambaye alidaiwa kuwa mchawi hivyo Mzee Malipula hakupenda.
Hivyo jambo hili katika jamii zetu linajidhihirisha wazi pale wazazi waonapo mtoto anafanya vema, wanatumia fursa hii kuwabariki na kuwatakia mema katika maisha yao na siyo tu watoto hata jamii kwa ujumla ionapo mtu fulani anafanya vizuri basi humbariki.
Mwaafrika anaamini kuwa mchawi ana nafsi mbili yaani nafsi iliyotulia na nafsi inayotembea ambapo ipo katika makundi mawili kundi la ndoto (nafsi iliyotulia) na nafsi inayotembea ndiyo inayoweza kudhuru. Temples katika uchunguzi wa falsafa ya kiafrika amebaini hilo ambalo pia linajidhihirisha katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” Gusto alipoguswa mikono akiwa usingizini na mtu asiyeonekana ambaye ni Madoda;
“..usiogope Gusto ndimi Madoda mtumishi wa baba yako katika milki yake nimetumwa nije nikuchukue na nikuongoze huko wenzangu waliko……” (uk 18).
“…. Kweli hakuwa mwingine bali Madoda sura yake ilikuwa haijanitoka bado tangu tulipochunga ng’ombe pamoja…” (uk 19).
 Hivyo Madoda ni nafsi inayotembea na ndiyo yenye kumchukua Gusto wakati akiwa nyumbani kwao. Pia jambo hili hili linajitokeza katika riwaya ya “Nagona” ambapo tunakutana na nafsi inayotembea ambayo hudhuru na inajidhihilisha kama ifuatavyo;
“….nilishitukia napigwa viboko matakoni na mgongoni …nilipigwa viboko mfululizo lakini sikuweza kujitingisha…..”(uk 1).
Hapa ni nafsi inayotembea ambapo mtu anapigwa kiboko kichawi bila mtu kumwona. Hali kadharika katika jamii zetu jambo hili lipo mfano katika kabila la wabena (Njombe) mtu anayedhaniwa kuwa ni mchawi ukienda kumuuangalia usiku wa manane hata ukimshitua kwa nguvu mtu yule huwa haamuki lakini baada ya muda mtu yule akiamka husema nilikuwa nimesafiri, hivyo hii wazi kuwa ipo nafsi inayotembea na nafsi tuli.
Mwaafrika anatawaliwa sana na suala la ukarimu na ushirikiano katika shida na raha, Temples anaamini kuwa waafrika wamekuwa na ukarimu na ushirikiano hasa pale jirani ama ndugu yake anapopatwa na tatizo kama vile (msiba, ajali) na mengine yamfanyayo mtu kuwa na huzuni au kama kuna tukio la furaha kama vile kufanikiwa kitu fulani, arusi, jando na unyago, sherehe za kuhitimu shule na sherehe nyinginezo ambazo bado zinamfanya mtu awe mwenye furaha. Katika mambo hayo yote waafrika wanakuwa wakarimu pia hata kushirikiana ili kuhakiki jambo lile linafanikiwa, hivyo jambo hili limejidhihilisha katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kama ifuatavyo;
“…..msichana mdogo aliyekuwa anazungumza na mama “kamwene binti yangu… habari gani zikuletazo asubuhi hivi?....(uk 49).
                “…mimi nakwenda huko kwenye kilio labda nitarudi tu jioni kuchukua matandiko..” (uk 50).
Bado wazo hili linajidhihirisha katika riwaya ya “Nagona” ambapo Mzee wakati anamkaribisha msanii na hii ndiyo inayoendelea kuthibitisha kuwa waafrika wanaukarimu.
“….karibu karibu karibu uketi. Tumekuwa tukikusubiri,” sauti ilitoka katikati ya mwanaga wewe mwenyewe” ahsante…(uk 14)”.
Hivyo kama ambavyo yamedhihirishwa katika riwaya zote mbili yaani Mirathi ya hatari na Nagona inasawili katika jamii zetu za kiafrika kwani waafrika hushirikiana na kuwa wakarimu katika shida na raha pale litokeapo tukio la furaha ama la huzuni kwa ndugu au jirani.
Mwaafrika hasahau jadi au asili hata kama ana elimu ya kimagharibi na kimashariki. Utafiti huu wa Temples katika suala hili ni kweli kwani licha ya kuwa mtu ana elimu ya juu kabisa ya kimagharibi yaani katika shahada ya kwanza, shahada ya uzamili pia shahada ya uzamivu bado akilejea kule alikozaliwa hufuata mila na taratibu zilizopo katika jamii husika bila kwenda kinyume, mfano katika makabila kama ni msukuma akirudi alikozaliwa huongea kisukuma na kama mnyakyusa hali kadharika. Na pia licha ya mtu kuwa na elimu hiyo bado anaamini nguvu za sihiri na hii imejidhihirisha katika riwaya ya “Mirathi ya hatari” ambapo mwandishi amemtumia mhusika Gusto ambaye alikuwa ana elimu hiyo lakini bado anaamini kuwa hirizi ndiyo yenye kumfanikisha kufaulu mitihani;
            “…baba yako ni mchawi na hiyo hirizi uliyoivaa ni ya madawa ya kufaulu mitihani…(uk 6).”
Pia jambo hili linajitokeza katika riwaya ya “Nagona” ambapo mwandishi amemtumia mhusika Mkombozi wa pili pamoja na kuwa msomi lakini aliwafuata wazee wa mila ili kuleta ukombozi mbali na elimu aliyokuwa nayo ya kimagharibi;
“…nilipomkaribia niliinua tena mikono yangu…(uk 37)”
Kwahiyo basi ni hili lipo hata kwa sisi japo tuna elimu ya kimagharibi lakini hatuzipuuzi mila na desturi za kule tulikotoka.
Kila mtu ana chembe za nguvu hai yaani inayomwezesha kutenda mambo yake na chembe hai ya kike ni kubwa zaidi kuliko ya kiume. Uchawi ni nguvu hai watu hutumia kupatia vyeo, ushindi na hata vita, lakini nguvu hai inaweza kuboresha au kufifiza katika utendaji wa mambo. Mfano, matumizi ya hirizi na kupiga lamri ni kuongeza nguvu hai. Hivyo jambo hili limejitokeza katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” ambapo Gusto amekuwa akitumia hirizi aliyopewa na mama yake ili kujikinga na maovu kijijini na hata wakati mwingine kuitumia ili kuweza kufanikisha kuyafanya masomo yake kwa ustadi wa hali ya juu, kwani utumiaji wa hirizi ndio umemfanya Gusto asidhurike na maovu ya kijijini;
“…ni kweli kwamba nilikuwa navaa hirizi; hirizi niliyopewa na mama kama kinga ya maovu kijijini.(uk 6).
“….wengine tulipochoka yeye alikuwa kama vile ndiyo kwanza anaanza. Hata leo bado nashangaa nguvu zile alizipata wapi….” (.Uk 5)
Pia katika riwaya ya “Nagona” ambapo mhusika Mimi anaonekana ana chembe nguvu hai zilizomwezesha kuyashinda mambo makubwa kama ya kishirikina na kichawi yaliyomkabili katika safari yake (uk 1-3).

Hivyo basi nukuu hizi inaonesha namna waafrika wanavyoamini nguvu za sihiri katika kuyashinda mambo hata yawe magumu ama mepesi hirizi na lamri ndiyo mshindi wao katika kuyatatua kwani ndio aliyeyafanya mambo hayo yawepo hapa dunia. 

No comments:

Post a Comment