Saturday, 2 January 2016

Dhana ya Lugha, Sifa za lugha, Tabia za lugha, Matumizi na umuhimu wa lugha

B. F. KIWALE
P.O BOX 774
IRINGA


© Kiwale, F. Brasto 2015


ISBN 9976 911 49 1




chapa ya kwanza 2015, December. 28.

Haki zote zimehifadhiwa. hakuna sehemu ya kazi hii itakayo ruhusiwa kuirudia kuitengeneza, kwa namna yoyote ile, bila ruhusa ya mwandishi au B. F  Consult P.O. Box 774, IRINGA.




Printing and publishing consultancy by
KAD Associates/ TFC, P.O Box 32746,
Dar es Salaam, Tanzania.













1.0  Utangulizi
1.1. Dhana ya Lugha.
Wataalamu mbalimbali wametoa ufafanuzi kuhusu dhana ya Lugha kama ifuatavyo.

Trudgil, (1974) anasema “Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.”

Sapir, (1921) anasema “Lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie  kuwasilishia mawazo,  maoni na mahitaji” mfumo huu hutumia ishara ambazo  hutolewa kwa hiari.

Weber, (1985) anasema  “Lugha ni mfumo wa mawasiliano ya mwanadamu ambao hutumia mpangilio  maalumu wa sauti kuunda vipashio vikubwa zaidi  kwa mfano mfano mofimu, maneno na sentensi” pia anadai kuwa lugha ni mfumo wowote wa mawasiliano ya  watu kwa mfano lugha ya kifaransa na lugha ya kihindi.

TUKI, (1990) masema “Lugha ni mfumo wa sauti zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.”

Todd,  (1987) anadai kuwa” lugha ni mfumo wa ishara za sauti ambazo kwazo watu huwasiliana.”

Barber, (1979) anaeleza kuwa “Lugha ni utaratibu wa kupeana habari unaotumia alama za sauti na  unaotumiwa na kundi fulani la watu kwa nia ya kuwasiliana na kushirikiana katika jamii.”

Cook (1969)  naye anasema” lugha ni mfumo wa sauti na ishara za kisarufi zinazotumika kuwasiliana na kupokezana utamaduni.”

Wataalamu hawa wote wanaelekea kukubaliana kuwa Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano baina yao.

Kwa ujumla Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa na watu wenye utamaduni unafanana ili kuwasiliana.

1.2.  Sifa za lugha
Lugha ina sifa zake kama zifuatazo; Lugha lazima imuhusu mwanadamu, lazima iwe na sauti ambazo hutamkwa kutoka kinywaji mwa mwanadamu, lugha hufuata mpangilio wa vipashio unaoleta maana, lugha ina sifa ya kujizalisha na pia lugha ina sifa ya kusharabu.

1.3.  Tabia za lugha
Pia lugha ina tabia zake kama zifuatazo; Lugha ina tabia ya kukua kutokana na jinsi inavyoendelea  kutumiwa na jamii, Lugha ina tabia ya  kuathiri na kukubali kuathiriwa kutokana na mwingiliano wa Lugha.

1.4.  Matumizi na umuhimu wa lugha
Lugha ina matumizi na umuhimu wake katika jamii kama vile, kutumika kuwasiliana, kuunganisha jamii, kujenga jamii, ni  chombo kinachoweza kuliifadhi na kueneza amali za jamii pia lugha  ni utambulisho wa jamii fulani.

1.5.  Dhana ya utambulisho
Utambulisho ni ubainisho unaomdhihirisha mzungumzaji Fulani kuwa yuko tofauti na  mzungumzaji mwingine au jamii Fulani iko tofauti na nyingine.

Utambulisho wa  mzungumzaji ni upekee alionao mzungumzaji katika kutumia Lugha yake utambulisho wa jamii ni ule upekee wa jamii.  Anaobainishwa kwa misingi ya kiutamaduni ambayo iko tofauti na misingi ya tamaduni  za jamii nyingine.

Utambulisho wa mzungumzaji huweza kubainishwa, kwa kutumia vibainishi vya kijamii na kiisimu. Vibainishi vya kijamii ni vibainishi ambavyo hufungamana na utamaduni wa jamii ya mzungumzaji na vibainishi vya kiisimu ni vibainishi vinavyohusu Lugha ya mzungumzaji

1.6.  Vibainishi vya kiisimu
Vifuatavyo ni vibainishi vya kiisimu vinavyothibitisha utambulisho halisi wa  mzungumzaji unaokubalika na yeye  mwenyewe pamoja na jamii yake. vibainishi hivyo ni  kama vile mkazo, lafudhi, kiimbo, lahaja, matamshi  ya sauti, maneno na hata miundo ya lugha
Mkazo, ni kipengele cha kiisimu kinachohitajia unguvunguvu wakati wa utamkaji mkazo ni kibainisho cha kiisimu ambacho kinaweza kumtambulisha mzungumzaji.  Mfano; Katika Kiswahili mkazo unatokea katika silabi ya pili kutoka mwisho mwa neno mfano katika neno “mama mdogo   mkazo upo kwenye silabi ya pili kutoka mwishoni .  Pia katika maneno ya kiingereza mkazo hutokea katika silabi ya mwanzoni mwa neno. Mfano neno “Baby sit katika neno hili  unguvunguvu umetokea katika silabi ya kwanza,   hivyo mkazo ni kibainisho cha kiisimu kinachoweza  kumtambulisha mzungumzaji.

Lahaja  ni vilugha vidogo vidogo vya Lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia lahaja za lugha moja zatofautiana katika matamshi, miundo ya sarufi na msamiati Mfano: Lugha za Kiswahili hutofautishwa kulingana na maeneo yake kama; kiamu (Kisiwani kwa lamu), kimvita (mjini mombasa), kiunguja (kisiwani Zanzibar). Pia hata lugha ya kiingereza ina lahaja mbalimbali na lahaja zake zinavyozungumzwa ni tofauti mfano; uingereza, marekani, uhindi, Australia na maeneo mengine./

Kiimbo ni hali ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti mtu anapozungumza. kiimbo husaidia kuleta maana kamili ya sentensi iliyokusudiwa. Mfano kama ni swali  mshangao au maelezo.

Mfano:  Dada amekuja? (swali)
              Dada amekuja. (Maelezo)
              Dada amekuja!  (mshangao)

Lafudhi ni namna ya uongeaji wa kitarafa au ni namna ya mtu ya kuyatamka maneno ambayo humtambulisha mahali anakotokea mfano, mtu wa Arusha huwa na lafudhi tofauti na mtu wa Makete.

Matamshi ya sauti, matamshi ndio humbainisha msemaji kuwa lugha yake ya kwanza ni ipi.
Mfano wapare wameathirika sana na lugha mama hivyo hushindwa kutofautisha kati ya “s” na “th” husema “thatha” badala ya “sasa.” Pia wanyakyusa  hushindwa kutofautisha kati ya “v” na “f” husema “fiatu fyangu”  badala ya “viatu vyangu” Hivyo matamshi ya sauti huweza kumtambulisha mzungumzaji.

Miundo ya lugha, mzungumzajji huweza kutambulishwa kwa miundo ya lugha, kwa mfano katika lugha ya kinyamwezi na kimatendo kama  wanaongea na mtu wanayemheshimu wanatumia uwingi badala ya umoja hata kama mtu anayeongea naye yupo mmoja tu.
Mfano:  “Mtafika saa ngapi?” badala ya  “Utafika saa ngapi?”

1.7.  Vibainishi vya kijamii
Baadhi ya vibainishi vya kijamii vinavyothibitisha utambulisho halisi wa mzungumzaji unaokubalika na yeye mwenyewe pamoja na jamii yake ni mavazi, chakula, utamaduni, mila na desturi, lugha, historia ya jamii imani

Chakula hiki ni kibainishi cha kijamii kinachothibitisha utambulisho halisi wa mzungumzaji kwa mfano: “Ndizi” ni chakula kinachopendwa sana na wanyakyusa  wachaga na wahaya, vilevile  viazi mviringo ni chakula kinachopendwa sana na  wakinga. Hivyo chakula huweza kumbainisha mzungumzaji.

Lugha, huweza kuutambulisha mzungumzaji kuwa ni wa jamii gani, mfano ukimwona mtu anazungumza lugha ya kikinga basi unajua kuwa huyu ni mtu wa makate au ukimwona mtu anazungumza kihaya unajua kuwa huyo ni mtu wa Bukoba, vilevile ukimwona mtu anazungumza kimasai basi utajua kuwa huyo mtu ni mmasai.

Mavazi, haya pia ni kibainisho halisi cha mzungumzaji, mfano; vazi la kimasai, kama mtu amevaa vazi la kimasai ukimwona utamtambua kwa vazi lake kuwa huyu ni mmasai, pia hata ukimwona mtu kavaa buibui utajua kuwa huyu ni muislamu, au ukimwona mtu kava vazi la kinaijeria utajua kuwa huyu ni mnaijeria. Hivyo mavazi nayo ni kibainisho cha kinachoweza kumbainisha mzungumzaji.

Mila na desturi, ni utaratibu na kanuni katika jamii fulani. Katika jamii zetu kila jamii ina utaratibu na katuni zake katika mfumo mzima wa maisha. Mfano. Kabila la wakinga wana utaratibu wao, mfano, mdogo anapomsalimia mtu mkubwa lazima apige magoti wakati baadhi ya jamii zingine hazina huo utaratibu. Hivyo basi ukiwaona watu wanasalimiana huku wakipiga magoti utawatambua kuwa watu hawa ni wa jamii fulani kulingana na mila na desturi zao.


2.0.  Hitimisho.
Hivyo vibainishi vya kiisimu na vibainishi vya kijamii huthibitisha utambulisho halisi wa mzungumzaji unaokubalika na yeye mwenyewe pamoja na jamii yake kwa ujumla.











 3.0.  MAREJEO.
Besha,  R.  (1994), Utangulizi wa lugha na isimu, Dar  es salaam University Press.
Habwe, J.  na  Karanje, P. (2004), Misingi ya sarufi ya kiwahili Nairobi Phonix Publishers.
Massamba, D. na wenzake (2004), Fonolojia ya Kiswahili sanifu (fokisa)  sekondari na vyuo TUKI

















6 comments: